RAIS DKT. SAMIA AMEWAJENGEA WANAWAKE MOYO WA UJASIRI NA KUJIAMINI

 





Singida, Septemba 9, 2025

Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Urais kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka historia mpya kwa kuimarisha nafasi ya mwanamke katika jamii, siasa na maendeleo ya taifa.

Akihutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza katika uwanja wa Bombadia, Singida Mjini, Dkt. Bashiru alisema kwa muda mrefu historia ya siasa duniani imekuwa ikimfanya mwanamke kuonekana kama kiumbe wa daraja la pili, hali iliyopelekea ukosefu wa usawa wa kijinsia.

> “Kwa muda mrefu nafasi ya mwanamke imekuwa kama ya pili kana kwamba utu wake ni nusu. Lakini kupitia msimamo wa kifalsafa na kiitikadi wa CCM, usawa wa wanaume na wanawake si suala la hiari, ni suala la lazima,” alisema Dkt. Bashiru.

Aidha, aliongeza kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, kumekuwa na ongezeko kubwa la sera, miradi na maamuzi yaliyoboresha maisha ya wanawake, na kuimarisha nafasi yao katika jamii.

> “Katika kipindi ambacho Dkt. Samia ameingia madarakani kama Rais na Mwenyekiti wa CCM, tazameni kitakwimu namna maamuzi, sera na utekelezaji wake ulivyoinua hali za akina mama. Si upendeleo, bali kuwajengea uwezo wa ujasiri, kufanya kazi na kujiamini,” alisisitiza.

Wananchi wa Singida walijitokeza kwa wingi kumpokea na kumsikiliza Rais Dkt. Samia, ambapo viongozi wa chama na wananchi waliendelea kuonesha mshikamano wa pamoja katika kumuunga mkono kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

🔖 Vyanzo vya habari: Hotuba ya Dkt. Bashiru Ally, mkutano wa hadhara wa CCM – Singida.



Post a Comment

0 Comments