TAWA Yamnasa Simba Mla Mifugo Kondoa

 




📍 Jitihada zaendelea kuwasaka simba wengine

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imefanikiwa kumkamata simba jike akiwa hai, kufuatia mfululizo wa mashambulizi yaliyosababisha zaidi ya mifugo 20 kuuawa katika Wilaya ya Kondoa, mkoa wa Dodoma.

Simba huyo alinaswa usiku wa Septemba 6, 2025 majira ya saa 4 usiku katika Kijiji cha Chemchem, baada ya msako mkali wa siku tatu ulioendeshwa na askari wa TAWA kwa kutumia mitego maalum.

Mashambulizi ya simba yameripotiwa katika Vijiji vya Chemchem na Iyoli, Kata ya Kingale, ambapo katika nyakati tofauti waliua ng’ombe wawili na punda mmoja, kisha baadaye kuua ng’ombe 18 katika gereza la King’ang’a pamoja na mbuzi wawili katika Kijiji cha Iyoli.

Kutokana na ongezeko la matukio hayo, TAWA ilianzisha operesheni ya kudhibiti wanyama hao, ikihusisha pia timu ya madaktari wa wanyamapori. Hatimaye, simba huyo alikamatwa kwa mbinu za kitaalamu.

Afisa Mhifadhi Daraja la Kwanza na Daktari wa Wanyamapori, Masalu Makoye Mroje, amesema simba huyo atasafirishwa kwenda eneo salama lenye mazingira rafiki, ili kuzuia madhara zaidi kwa wananchi na mifugo yao.

Wananchi wa Kijiji cha Chemchem wameipongeza Serikali kupitia TAWA kwa kuchukua hatua madhubuti katika kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali.

“Tumekuwa na changamoto ya wanyama wakali na waharibifu kwa muda sasa. Simba walitula mifugo na kutusumbua, lakini leo amani imerejea baada ya TAWA kufanikisha kumdhibiti simba huyo. Pia wametuahidi kufuatilia simba wengine ili kuwaondoa katika kijiji chetu,” alisema Mwenyekiti wa Kijiji cha Chemchem, Bw. Mashaka Said Funga.

Aidha, TAWA imeendelea na uchunguzi na ufuatiliaji ili kubaini kama kuna simba wengine bado wapo katika maeneo hayo, na kuwaomba wananchi kutoa taarifa mapema iwapo watawaona.



Post a Comment

0 Comments