Mkurugenzi wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Richard Kayombo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni ya Tuwajibe
Na mwandishi wetu
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imezindua rasmi kampeni kwa jina la “Tuwajibike” ambayo itakuwa endelevu kuanzia mwezi huu.
Akitambulisha kampeni hiyo kwa waandishi wa habari leo Mei 2, 2023 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Richard Kayombo amesema kampeni hiyo ina malengo makuu matatu.
Ametaja malengo hayo kuwa ni pamoja na kuwakumbusha na kuwahamasisha wauzaji wa bidhaa na watoa huduma nchi nzima kuwajibika kwa kutoa risiti halali ya EFD kila wauzapo bidhaa au kutoa huduma.
Malengo mengine ni kuwakumbusha na kuwahamasisha wanunuzi wa bidhaa na huduma kote nchini kuwajibika kudai risiti halali za EFD pamoja na kuzikagua ili kujiridhisha kuwa zinakidhi vigezo vyote muhimu.
Kayombo ameongeza kuwa itahusisha pia ufuatiliaji wa utoaji wa risiti halali za EFD nchi nzima pamoja na kuchukua hatua kwa wauzaji wasiofuata Sheria katika utoaji wa risiti halali za EFD.
"Zikiwemo kutotoa risiti ya EFD, kutoa risiti yenye mapungufu kama kuwa na kiwango cha chini kulingana na thamani halisi ya bidhaa au huduma, kutoa risiti moja ya kusindikiza mizigo, kufanya biashara ya kuuza risiti pasipokuwa na biashara yoyote," amesema Kayombo na kuongeza,
“Risiti halali ya EFD inatakiwa kukidhi vigezo vikuu vinne (4) ambavyo ni jina la biashara,tarehe halisiya mauzo,kiasi halisi cha pesa kilichonunuliwa bidhaa au TIN ya mnunuzi au vyote kwa pamoja.
Kwamba adhabu itatolewa kwa atakayebainika kufanya udanganyifu ambapo kwa mfanyabiasha atakayebainika kutokutoa risiti halali ya EFD au kufanya udanganyifu atatozwa faini ya Shilingi milioni 3 hadi shilingi milioni 4.5 au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja.
Aidha kwa mteja ambaye atabainika kufanya udanganyifu kwa kutodai Risiti atapigwa faini ya kuanzia shilingi 30,000 hadi shilingi milioni 1.5 au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja.
0 Comments