SERIKALI YATOA KIFUTA JASHO NA KIFUTA MACHOZI CHA ZAIDI YA TSHS. MILLIONI 399 KWA WANANCHI WALIOATHIRIWA NA TEMBO NACHINGWEA

 





Na. Beatus Maganja


SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa kifuta jasho na kifuta machozi  cha zaidi ya shillingi millioni 399 kwa  wananchi 1,658 walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu katika wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi.


Kauli hiyo imetolewa Aprili 09, 2024 na Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mhe. Mohamed Hassan Moyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ziara ya kuelezea jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu, ziara iliyofanywa na TAWA Mkoani humo.


" Serikali kupitia utaratibu wake wa kifuta jasho na kifuta machozi, wahanga zaidi ya 1658 kwenye wilaya ya Nachingwea walipatikana lakini fedha ambazo Dkt. Samia Suluhu Hassan kazileta kwa ajili ya kifuta jasho Mwaka jana ni shillingi 399, 405,000/= na wale wote ambao waliokuwa wanastahili kupata kifuta jasho waliweza kukipata kifuta jasho hicho" alisema Mhe. Moyo


Mhe. Mohamed Moyo amesema wilaya yake imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo wanaoathiri mali na maisha ya wananchi  lakini pamoja na changamoto hizo amekiri  kuwepo na jitihada nyingi zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA na TAWIRI katika kuelimisha wananchi mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori pamoja na kuwadhibiti.


"Jitihada za TAWA zimefanyika mara nyingi na mimi mwenyewe nimekuwa nikishiriki, jitihada moja ni kwa kutumia helikopta katika kuwaswaga au kuwafukuza wanyama tembo" alisema Mkuu huyo wa wilaya


Akibainisha jitihada zilizofanywa na TAWA Katika kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu Kanda ya Kusini Mashariki Mhifadhi Mkuu Kitengo cha Oparesheni Linus Chuwa amesema TAWA imeanzisha vituo 10 vya Askari wa kukabiliana na wanyamapori hao ambapo vitano kati ya 10 ni vya kudumu  na vingine  vitano ni vya muda mfupi hasa pale matukio ya wanyamapori hao yanapojitokeza.


TAWA pia imefanikiwa kununua gari jipya katika kituo cha malola ambalo hutumiwa na Askari wa kituo hicho, pia imenunua ndege nyuki (drones) maalumu kwa ajili ya kufukuzia tembo ambazo zilitumika katika zoezi la kufukuza tembo mwaka jana (2023), zoezi ambalo linatajwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.


Jitihada zingine zilizofanywa na TAWA kwa kushirikiana na wadau ni pamoja na kuwafunga visukuma mawimbi tembo watatu ambao ni  viongozi wa makundi  na hivyo kufuatilia mienendo yao ili kuwadhibiti kabla hawajafika katika makazi ya binadamu.


Mhifadhi Mkuu Linus Chuwa ameongeza kusema  TAWA  imepeleka Askari wa wanyamapori wa vijiji 41 (VGS)  katika chuo cha Likuyu Sekamaganga kwa ajili ya kupatiwa elimu ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu na amethibitisha kuwa Askari hao hutumiwa na TAWA Katika matukio mbalimbali ya kudhibiti wanyamapori hao 


Kwa upande wake, Afisa habari wa TAWA Beatus Maganja amesema lengo kuu la ziara hiyo Mkoani humo ni kuelezea jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA Katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu na kuwahakikishia wananchi kuwa TAWA iko kazini kuhakikisha inafanya Kila iwezalo kuwadhibiti wanyamapori hao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile TAWIRI, GIZ na TANAPA.






Post a Comment

0 Comments