MALKIA WA NGUVU 100 KUPELEKWA CHINA KUJIFUNZA BIASHARA.




 Na mwandishi wetu

Clouds Media Group kupitia Malkia wa Nguvu imesema kuwa mwaka huu 2025 imepanga kupeleka Malkia wa Nguvu 100 Nchini China kwa ajili ya  kujifunza teknolojia, Viwanda na Masoko mapya.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kamati ya Malkia wa Nguvu, Liliane Masuka kwenye kilele cha tuzo za Malkia wa Nguvu 2025 zilizofanyika Jijini Dar es salaam na kuelezea mipango mingine ya Malkia wa Nguvu 2025 ikiwemo mradi wa Mai Shop (Malkia Digital Hub ) ambao ni jukwaa la kidijitali kwa wanawake kupata maarifa, masoko na mitandao.

Jambo lingine ni Kipepeo Seed Fund ambao huu ni mfuko wa kusaidia wasichana wanawake wabunifu kupata mitaji ya biashara.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Doto Biteko ameipongeza Clouds Media Group kwa kutengeneza jukwaa hili ambalo limekua likitoa Malkia wa nguvu wanaoanzia chini mpaka kuwa Wafanyabiashara wakubwa kwa miaka tisa mfululizo.

'Naomba pia, kutumia fursa hii kuwapongeza Menejimenti ya Clouds Media kwa kuanzisha na kuendeleza Jukwaa hili la ‘Malkia wa Nguvu. Tangu kuanzishwa kwake, hadi sasa, jukwaa hili limekuwa ni chachu kubwa ya maendeleo kwa wanawake na jami kwa ujumla. Kwa kweli tunatambua na tunathamini jitihada zenu' - Mhe. Doto Biteko.

Kwa upande mwingine Mhe. Doto Biteko amesema kwa Nchi yetu tumepiga hatua kubwa kwenye kuzikabili changamoto za Wanawake nchini.

'Tanzania tumefanikiwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake kijamii na kiuchumi. Pia tumepiga hatua kubwa ya kuhakikisha kuwa Mwanamke anakuwa ni sehemu ya Maendeleo katika Jamii. Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na Fursa za elimu, Mazingira wezeshi ya kiuchumi, Fursa za biashara, uwekezaji na fursa za kifedha (mikopo yenye masharti nafuu). Ushirikiano na Jumuiya ya Kimataifa Mashirika kama UN Women, UNESCO, na UNICEF, Huduma bora za kiafya Afya ya Mama na Mtoto, Huduma za Maji safi na Nishati ya kupikia, Hivyo kurahisishia maisha ya mwanamke' - Mhe. Biteko.

Clouds Media Group kupitia Malkia wa Nguvu imetoa tuzo 10 kwa Wanawake waliofanya vizuri sekta mbalimbali, ambapo Washindi hao ni pamoja na Tulia Ackson (Spika wa Bunge la Tanzania na Rais wa Mabunge Duniani) ambaye kashinda tuzo ya Heshima, Marina Njelekela aliyeshinda tuzo ya afya na ustawi wa jamii, Happiness Nyiti aliyeshinda kipengele cha Kilimo Biashara, Kipengele cha utumishi wa umma kashinda Mhandisi Zena Ahmed Said na Washindi wengine wengi. 

Tuzo za Malkia wa nguvu 2025 zinatarajia kwenda Kanda 5 za Nchi ya Tanzania ambazo ni Kanda ya ziwa, Kanda ya kaskazini, kanda ya kati na Kanda ya Nyanda za Juu kusini.






Post a Comment

0 Comments