Dar es Salaam, Mei 14, 2025
Katika hatua ya kuimarisha ushirikiano na kukuza uelewa ndani ya sekta ya madini nchini Tanzania, Chama cha Tanzania Mining Supplies Association (TAMISA) kinatarajia kuzindua rasmi jukwaa lake jipya sambamba na kongamano maalum litakalobeba mada kuu: “Nafasi ya Mtanzania katika Sekta ya Madini.” Tukio hilo litafanyika Mei 16 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kuhusu uzinduzi huo, Sebastian Ndege amesema kuwa jukwaa hilo limebuniwa kwa lengo la kuwaunganisha wadau wote wa sekta ya madini, hususan wauzaji wa vifaa, ili kuwa na sauti ya pamoja katika kukuza taaluma, uelewa na ubunifu ndani ya sekta hiyo nyeti.
“Tunatambua kwamba sekta ya madini ni uti wa mgongo wa maendeleo ya kiuchumi nchini, lakini bado kuna pengo kubwa la mawasiliano na uelewa miongoni mwa wadau mbalimbali. Kupitia TAMISA, tunakusudia kulijaza pengo hilo kwa kuwa na jukwaa la majadiliano, ushirikiano na elimu endelevu,” amesema Ndege.
Katika siku hiyo ya uzinduzi, TAMISA itashuhudia matukio matatu muhimu: kuzinduliwa kwa kamati rasmi ya chama, kufanyika kwa kongamano lenye mada kuu kuhusu nafasi ya Mtanzania katika sekta ya madini, na kutambulishwa rasmi kwa jukwaa hilo jipya la majadiliano na elimu.
Mwenyekiti wa TAMISA, Peter Andrew, amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni kuhakikisha kuwa sauti ya Mtanzania haipotei katika sekta ambayo kwa muda mrefu imeonekana kutawaliwa na maslahi ya nje.
“Tunataka kujenga uelewa wa pamoja. Kupitia jukwaa hili, watu wote wanaofanya kazi katika sekta ya madini – kuanzia wauzaji wa vifaa, wachimbaji, wasafirishaji hadi wadau wa sera – watakuwa na mahali pa kupata taarifa sahihi, kushiriki mijadala yenye tija na kujifunza kutoka kwa wataalamu,” amesema Andrew.
Ameongeza kuwa kongamano hilo na majukwaa yanayofuata yatakuwa sehemu ya mfululizo wa matukio ambayo yatalenga si tu kutoa taarifa, bali pia kuelimisha wadau kuhusu masuala mbalimbali yanayogusa sekta ya madini, yakiwemo mabadiliko ya sera, usalama kazini, teknolojia mpya, pamoja na fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.
Kwa mujibu wa TAMISA, taarifa zaidi kuhusu kongamano hilo, mada zitakazowasilishwa, pamoja na ratiba ya matukio, zinapatikana kupitia tovuti ya chama hicho. Wadau wote wametakiwa kufuatilia kwa karibu kwani jukwaa hili linatarajiwa kuwa kichocheo kikuu cha mabadiliko chanya katika sekta ya madini Tanzania.
0 Comments