AJALI MGODINI NYANDOLWA: WATANO WAOKOLEWA KATI YA 25 WALIOFUKIWA NA KIFUSI

 




Na mwandishi wetu

Juhudi za kuokoa mafundi waliokwama chini ya ardhi katika Mgodi wa Nyandolwa, wilayani Shinyanga, zimezaa matunda baada ya mafundi watano kuokolewa kati ya 25 waliokuwa wamefukiwa na kifusi kufuatia kutitia kwa ardhi mnamo Agosti 11, 2025.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro amesema, tukio hilo lilitokea katika eneo la leseni ya uchimbaji inayomilikiwa na Kikundi cha Wachapakazi, katika Kijiji cha Mwongozo, Kata ya Mwenge, ambapo mafundi 25 walikuwa wakitekeleza shughuli za ukarabati wa mashimo matatu tofauti (maduara) kabla ya ajali hiyo kutokea.

Mtatiro amethibitisha kuwa, hadi sasa mafundi watano wameokolewa, mmoja kati yao alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu, na mmoja mwengine amepatikana wakiwa tayari amefariki na watatu walitolewa wakiwa hai. Zoezi la uokoaji linaendelea kwa mafundi waliobaki.

“Tunaungana na familia zilizopoteza wapendwa wao katika kipindi hiki kigumu. Serikali iko pamoja nanyi na tutaendelea kufuatilia na kusaidia kikamilifu juhudi za uokoaji hadi tukio hili litakapomalizika,” amesema Mtatiro.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Madini, Sehemu ya Uendelezaji Uchimbaji Mdogo wa Madini, Mhandisi Moses Kongola amesema ameishukuru Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Kampuni ya Barrick Bulyanhulu kwa juhudi wanazoendelea kuzionesha za kuhakikisha mafundi wote waliokwama chini ya ardhi katika mgodi huo wanapatikana.

Pia, Mhandisi Kongola amesisitiza usalama mahala pa kazi ambapo amewataka waokoji wote kuzingatia usalama katika kutekeleza shughuli hiyo.

“Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa mazingira ya kazi yanazingatia viwango vya usalama. Tutaendelea kusimamia hili kwa nguvu zote,” amesema Mhandisi Kongola.

Aidha, timu ya waokoaji imeiomba Serikali kuwapatia vifaa vya kisasa vya uokoaji, ikiwemo glavu, maski za kuzuia vumbi (balakoo), reflector, na vifaa vingine vya kinga, ili kuongeza ufanisi na usalama katika zoezi hilo.

Naye, Mkuu wa Ukaguzi Migodi, Mhandisi Khamisi Kamando amesisitiza kuwa, serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kuwa juhudi za uokoaji zinafanikiwa na hatua madhubuti zinachukuliwa kuimarisha usalama wa wachimbaji wadogo nchini.








Post a Comment

0 Comments