Dorcas Mwilafi Achukua Fomu ya Ubunge Kawe Kupitia CHAUMMA

 





Na mwandishi wetu

Mgombea ubunge kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Bi. Dorcas Francis Mwilafi, ameonesha dhamira ya kuleta mabadiliko katika Jimbo la Kawe baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo leo tarehe 15 Agosti 2025. Hatua hiyo imefanyika katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ambapo alipokelewa na viongozi wa chama hicho pamoja na wafuasi wake.

Bi. Mwilafi amesema ameamua kugombea nafasi ya ubunge kwa lengo la kuwakilisha wananchi wa Kawe kwa uwazi, uwajibikaji na uadilifu, huku akiahidi kushirikiana nao katika kupanga vipaumbele vitakavyoliletea jimbo hilo maendeleo endelevu. “Ninakuja kama mkombozi wa wananchi wa Kawe. Sauti ya kila mmoja itasikika, na kila senti ya maendeleo itatumika ipasavyo kwa manufaa ya wote,” alisema.

Viongozi wa CHAUMMA waliokuwepo kwenye hafla hiyo wamempongeza kwa ujasiri na kujitolea kwake, wakisema kuwa chama kimejipanga kuhakikisha kinatoa wagombea wenye maono makubwa na misimamo thabiti ya kulinda maslahi ya wananchi. Waliwahimiza wakazi wa Kawe kujitokeza kwa wingi kumpa kura ili kuweka msingi mpya wa maendeleo na uwajibikaji.

Aidha, wananchi waliohudhuria tukio hilo walieleza matumaini yao kwamba mgombea huyo ataweza kuondoa changamoto za muda mrefu zinazolikabili jimbo la Kawe, ikiwemo miundombinu duni, huduma za kijamii zisizokidhi viwango na ukosefu wa ajira kwa vijana.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unatarajiwa kufanyika Oktoba, ambapo vyama mbalimbali vinaendelea kuwasilisha majina ya wagombea wake kwa nafasi za urais, ubunge na udiwani kote nchini. Hatua ya Bi. Dorcas Mwilafi kuingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge Kawe imezidisha ushindani na hamasa kwa wapiga kura katika jimbo hilo.

Post a Comment

0 Comments