Dar es Salaam, Tanzania – 6 Agosti 2025 —
Wadau kutoka sekta za utalii, biashara, na serikali wamekutana leo katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, kushiriki katika Jukwaa la Wadau wa Sekta ya Utalii wa Mikutano Tanzania (MICE), tukio kubwa lililolenga kuimarisha sekta ya Mikutano, Safari za Motisha, Makongamano na Maonesho (MICE) nchini Tanzania.
Jukwaa hilo lilianza saa 8:30 mchana kwa hotuba ya ufunguzi iliyotolewa na mwakilishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, aliyesisitiza dhamira ya serikali katika kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha sekta ya Mikutano barani Afrika. Hii ni moja ya sehemu kuu zinazoiletea Tanzania watalii kutoka nje ya nchi, na kuingiza fedha za kigeni. Uwasilishaji kuhusu Mtazamo wa Sekta ya Utalii wa Mikutano (MICE) ulifuatia, ukitolewa na mwakilishi kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), ambapo alieleza mwenendo wa sasa wa soko, changamoto, na fursa zilizopo ndani ya nchi na ukanda wa Afrika Mashariki. Alitolea mfano wa ujenzi wa kumbi kubwa za mikutano zinazojengwa sehemu mbalimbali nchini, mfano wa jiji la Arusha ambapo ukumbi utakaoingia watu 5000 unajengwa.
Washiriki walipata fursa ya kupata mafunzo ya kitaalam kuhusu Uzingatiaji wa Sheria, Ununuzi na Mikataba, yaliyoendeshwa na taasisi ya UONGOZI, ambayo yalilenga kutoa mwongozo wa kiutendaji kuhusu taratibu na sheria katika uendeshaji wa biashara za mikutano na makongamano nchini.Miongoni mwa mambo muhimu ya jukwaa hilo ilikuwa Jopo la Majadiliano kuhusu Sera, Sheria na Kanuni za kuzingatia katika uendeshaji wa biashara kwenye Sekta ya Utalii wa Mikutano, lililowakutanisha wataalamu kutoka TTB, BASATA, TRA, na BRELA.
Mada kuu zilihusu kuboresha uratibu kati ya taasisi, kurahisisha taratibu za kibiashara, na kuvutia wawekezaji katika sekta hiyo.Vilevile washiriki waliohudhuria Event Management Masterclass kati ya mwezi Februari na Agosti, walitunukiwa Vyeti, kama ishara ya kutambua juhudi zao katika kupata maarifa ya kitaalamu kuhusu upangaji na usimamizi wa matukio.
Masterclass hizi zinatolewa na kampuni ya Popular Links kwa kushirikiana na wadau wengine.Tukio hili lilihitimishwa kwa Tafrija Mchapalo (Networking Cocktail Reception) kuanzia saa 12:00 jioni, ambapo washiriki walipata nafasi ya kuanzisha mahusiano ya kibiashara na kushirikiana katika miradi ya baadaye.
Jukwaa hili limeandaliwa na kampuni ya Popular Links, kwa ushirikiano na Alliance Française Dar es Salaam na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), na limepongezwa kwa kuwa hatua muhimu katika juhudi za kuikuza Tanzania kama kitovu cha sekta ya mikutano (MICE) katika ukanda wa Afrika.
Kwa Mawasiliano:📞 +255 764 781 856📧 admin@popularlinks.co.tz🌐 www.popularlinks.co.tz
0 Comments