TFS Yakabidhi Mbao zenye Thamani ya Milioni 10 kwa Ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Meru

 



Na mwandishi wetu

Na Mwandishi Wetu, Arumeru

*ARUMERU*. Serikali ya Wilaya ya Arumeru imepokea msaada wa vipande 896 vya mbao vyenye thamani ya shilingi milioni 10 kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) - shamba la miti Meru/Usa, kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya samani katika Hospitali ya Wilaya ya Meru.

Akizungumza leo Agosti 7, 2025 katika hafla ya makabidhiano ya msaada huo iliyofanyika hospitalini hapo, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Mwinyi Ahmed Mwinyi amesema msaada huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

“Leo tumeshuhudia TFS wakituunga mkono kwa vitendo, kwa kutuletea msaada huu muhimu wa mbao ambao utasaidia kutatua kwa asilimia 70 changamoto ya upungufu wa fenicha hospitalini. Hii ni hatua kubwa katika kukamilisha azma ya Serikali kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi,” alisema Mhe. Mwinyi.

Mkuu huyo wa wilaya alibainisha kuwa msaada huo wa mbao unakwenda kuongezea thamani katika uwekezaji mkubwa uliokwisha kufanyika katika hospitali hiyo, ambapo zaidi ya shilingi milioni 900 zilitolewa na Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa majengo mbalimbali ya hospitali hiyo, ikiwemo jengo la wagonjwa wa nje (OPD), bohari ya dawa, maabara, jengo la kuchomea taka pamoja na ununuzi wa mashine ya kisasa ya kuchomea taka za hospitali.

“Ni jukumu letu kama viongozi kuhakikisha mbao hizi zinatumika kwa lengo lililokusudiwa. Tunawaagiza viongozi wa afya na halmashauri kufanya tathmini ya gharama za kutengeneza samani zinazohitajika kwa kutumia mbao hizi, na Serikali ya Wilaya ipo tayari kuchangia asilimia 30 iliyobaki ili tufikie asilimia 100 ya mafanikio,” aliongeza Mhe. Mwinyi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Mwl. Zainabu Makwinya alishukuru TFS kwa kujibu maombi ya hospitali na kueleza kuwa msaada huo utasaidia kumalizia kikamilifu upungufu wa samani uliokuwa bado unaikabili hospitali licha ya kukamilika kwa majengo.

“Naishukuru Serikali Kuu kwa kutupatia zaidi ya shilingi milioni 900 ambazo zilitumika vizuri na kwa uadilifu mkubwa. Majengo yamekamilika na sasa kupitia msaada huu wa TFS, hospitali yetu itakamilika kwa asilimia 100,” alisema Makwinya.

Akizungumza kwa niaba ya TFS, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Meru/Usa, Ali D. Maggid alisema msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa bajeti  ya shamba inayolenga kusaidia jamii zinazolizunguka shamba.

“Shamba letu la miti lina ukubwa wa hekta 8,170 na linazungukwa na vijiji 32. Tumeweka utaratibu wa kusaidia miradi ya kijamii kila mwaka. Mwaka huu, tumeamua kusaidia Hospitali ya Wilaya ya Meru kwa kutekeleza ahadi tuliyotoa kutokana na changamoto ya samani iliyokuwa ikikabili hospitali hii,” alisema Maggid.

Aliongeza kuwa msaada huo wa mbao uliotolewa leo una thamani ya shilingi milioni 10 na unalenga kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha huduma za afya nchini.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Arumeru, Dkt.Fabian Weslous, alieleza kuwa mbao hizo zitasaidia kutengeneza fenicha mbalimbali zikiwemo meza, viti, mabenchi na pallets za kuhifadhia dawa, hatua ambayo itaongeza hadhi ya hospitali hiyo kufikia viwango vya hospitali za wilaya.

“Changamoto ya fenicha ilikuwa ni kikwazo kikubwa baada ya kukamilika kwa majengo. Kupitia msaada huu, tunaamini huduma zetu zitaimarika zaidi. TFS wamekuwa mshirika wa kweli na tunawaahidi kutumia mbao hizi kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema Dkt. huyo.

Wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya aliomba uongozi wa hospitali na halmashauri kuharakisha mchakato wa kutengeneza samani ili kusaidia huduma zianze kutolewa kikamilifu. Pia alisisitiza kuwa thamani ya fedha (value for money) izingatiwe katika kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo.











Post a Comment

0 Comments