MAJALIWA AFUNGUA KONGAMANO LA NNE LA KITAIFA LA UFUATILIAJI NA TATHMINI
Mwanza, Septemba 11, 2025 — Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amemuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano la Nne la Kitaifa la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (Monitoring, Evaluation & Learning) lililofanyika leo kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Malaika Beach, jijini Mwanza.
Kongamano hilo limewaleta pamoja wadau mbalimbali wa maendeleo, ikiwemo wakurugenzi wa halmashauri, wataalam kutoka sekta ya umma na binafsi, pamoja na viongozi na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika na nje yake. Lengo ni kuchochea mafunzo, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mbinu za ufuatiliaji na tathmini zitakazochangia utendaji bora wa miradi na maendeleo endelevu.
Kaulimbiu ya kongamano ni:
“Kuimarisha Uwezo wa Ufuatiliaji na Tathmini kwa Jamii ili Kuwezesha Utendaji Bora na Maendeleo Endelevu.”
Waziri Mkuu Majaliwa alisisitiza umuhimu wa kujenga uwezo wa kitaaluma kwa watendaji wa upande wa utekelezaji na ufuatiliaji, pamoja na kuunganisha mafunzo na sera ili matokeo ya tathmini yatumike kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Washiriki wanatarajia kujadili changamoto za sasa, njia za kuboresha ukusanyaji na matumizi ya data, pamoja na mikakati ya kuhamasisha utaalam wa ndani katika shughuli za M&E ili kutekeleza malengo ya maendeleo ya Taifa na Dira ya Taifa 2050.
0 Comments