WASIRA AWAPA UJUMBE MZITO WALIOONGOZA UBUNGE, UDIWANI


 

WASIRA AWAPA UJUMBE MZITO WALIOONGOZA UBUNGE, UDIWANI


Kilosa, Morogoro – 11 Septemba 2025

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amewataka wanachama wa CCM walioongoza kura za maoni na kupewa dhamana ya kupeperusha bendera ya chama katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kuendeleza mshikamano na umoja ndani ya chama badala ya kuleta mifarakano.

Amesema CCM ni kama mtumbwi unaosafirishwa na wote, hivyo haitavumiliwa kuona baadhi ya wanachama wachache wakitaka kutoboa mtumbwi huo na kuathiri maslahi ya chama na wananchi kwa ujumla.

Wasira alitoa kauli hiyo wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya wilaya hiyo, akiwa katika ziara ya kumnadi mgombea urais wa CCM, wagombea ubunge pamoja na wagombea udiwani.

Amesema anatambua kwamba katika baadhi ya maeneo kumeibuka misuguano kutokana na matokeo ya kura za maoni, ambapo baadhi ya waliopoteza walidai hawakushindwa kihalali. Hata hivyo, aliwahimiza washindi kuwa mstari wa mbele katika kuleta mshikamano.

> “Ninyi mliopewa dhamana ya kupeperusha bendera ya Chama, jukumu lenu ni kubwa zaidi la kuunganisha na kuleta mshikamano kuliko kuwafarakanisha wenzenu. Ukishinda halafu ukawa unatamba na kuwakejeli waliopoteza, unaleta mpasuko ndani ya chama,” alisema Wasira.

Amesisitiza kuwa ushindi wa kura za maoni ndani ya chama sio mwisho wa mchakato, bali ni sehemu ya mfumo wa kupata wagombea. Alifafanua kuwa wakati mwingine chama huamua kumpitisha mgombea wa pili au hata wa tatu, kulingana na vigezo vilivyowekwa.

> “Kumbukeni uongozi ni zamu kwa zamu. Leo umepewa nafasi, kesho ni ya mwingine. Hivyo, ni jukumu lenu kuhakikisha mshikamano unadumu, kwa sababu CCM ni kama mtumbwi tunaosafiria sote – hatuwezi kuukubali utobolewe na wachache,” aliongeza.

Aidha, katika ziara hiyo, Wasira alitoa wito wa kura kwa mgombea urais kupitia CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan, mgombea ubunge wa Jimbo la Kilosa Prof. Palamagamba Kabudi, mgombea ubunge wa Jimbo la Mikumi Denis Londo, pamoja na wagombea wa nafasi za udiwani katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Morogoro.











Post a Comment

0 Comments