Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele, leo Agosti 14, 2025 amemkabidhi rasmi mkoba wenye fomu za kuomba kuteuliwa kuwa Mgombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Mhe. Wilson Elias Mulumbe. Hafla hiyo imefanyika katika Makao Makuu ya Tume, jijini Dodoma.
Mhe. Mulumbe aliambatana na Mgombea Mwenza wake, Mhe. Shoka Khamis Juma, katika shughuli hiyo muhimu ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu. Wawili hao walipokelewa na viongozi waandamizi wa Tume, akiwemo Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ndg. Ramadhan Kailima, ambaye alishuhudia makabidhiano hayo.
Mwenyekiti Mwambegele aliwahimiza wagombea hao kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi wakati wa kujaza na kurejesha fomu hizo. Pia aliwataka kuendesha kampeni zenye amani na kuzingatia maadili ya kisiasa, ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa heshima na unaoendeshwa kwa misingi ya demokrasia.
Kwa upande wake, Mhe. Mulumbe alishukuru Tume kwa uratibu mzuri wa zoezi hilo na kuahidi kufuata masharti yote yaliyowekwa. Alisisitiza kuwa chama chake kimejipanga kuendesha kampeni zenye sera na hoja, zenye lengo la kuwaletea maendeleo Watanzania wote bila kujali itikadi zao za kisiasa.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inataraji kufanya uteuzi wa wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais Agosti 27, 2025. Baada ya uteuzi huo, kampeni rasmi zitafanyika kwa mujibu wa ratiba ya kitaifa hadi siku ya kupiga kura mwezi Oktoba.
0 Comments