Na mwandishi wetu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha maslahi ya walimu ili kuwaongezea motisha na mazingira bora ya kufundishia.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 14 Agosti 2025, baada ya kukizindua rasmi Chuo cha Ualimu cha Nkrumah kilichopo Mfenesini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ameeleza kuwa Serikali ina dhamira ya dhati na mikakati ya kuimarisha sekta ya elimu ili mafanikio yanayopatikana sasa ya ongezeko la ufaulu wa wanafunzi katika ngazi mbalimbali yawe ya kudumu.
Rais Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa azma ya kukirejesha chuo hicho, ambacho kilikuwa chimbuko la umahiri na uandaaji wa walimu bora Zanzibar, inalenga kuzalisha walimu wabobezi, weledi na wenye maadili katika ufundishaji.
Akizungumzia changamoto ya uhaba wa walimu, Dkt. Mwinyi amesema Serikali imetoa ajira mpya za ualimu 5,265 ili kupunguza changamoto hiyo.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya sekta ya elimu kwa kujenga skuli za kisasa, maabara, maktaba na dakhalia ili kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi kusoma katika mazingira bora.
Mapema, Rais Dkt. Mwinyi alizindua Mtaala maalum wa vyuo vya ualimu Zanzibar, pamoja na kupokea nishani maalum iliyotolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa heshima ya kumuenzi aliyekuwa Mkuu wa kwanza wa Chuo cha Ualimu Nkrumah, Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Akiwasilisha taarifa ya kitaalamu ya ujenzi wa chuo hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdullah Said, amesema mradi huo umegharimu shilingi bilioni 10.9 na umejengwa na kampuni ya kizalendo ya Quality Building Construction. Aidha, chuo kina uwezo wa kuchukua wanafunzi 810, kwa wastani wa wanafunzi 45 kwa kila darasa.
0 Comments